Maji ya mito yatajwa chanzo kikuu cha magonjwa ya mlipuko
12 February 2024, 15:12
Jamii Mkoani Kigoma imetakiwa kuzingatia usafi wa mazingira ili kujilinda na magonjwa ya mlipuko ambayo yamekuwa yakiwakumba baadhi ya wakazi wa mkoa huu katika baadhi ya maeneo ikiwemo kibirizi, Kalalangabo na Gungu lakini na wilaya ya Uvinza ambapo watu 74 waliugua ugonjwa huo kwa mwaka 2023 kuanzia mwezi February-Novemba na wagonjwa 2 walifariki.
Na, Josephine Kiravu.
Akizungumza na Radio Joy fm hivi karibuni Afisa afya Mkoani Kigoma Nesphory Songo amesema kumekuwa na visa vya wagonjwa ambavyo vimeripotiwa kwenye vituo vya afya huku chanzo kikuu kikitajwa kuwa ni matumizi ya maji ya vyanzo vya mito ambayo hayachemshwi wala kuwekewa dawa pamoja na uwepo wa taka zinazozagaa mitaani na kwenye vizimba katika maeneo ya masoko.
Ameongeza kuwa baadhi ya wakazi wa maeneo hayo hawana vyoo bora pamoja na uwepo wa mwingiliano wa raia kutoka nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Burundi.
Nao baadhi ya wakazi wa Kata ya kibirizi ambao pia ni wajasiriamali wamesema kukosekana kwa elimu ya namna ya kujilinda na kipindupindu pamoja na baadhi ya wananchi kukosa vyoo ni chanzo cha eneo hilo kukumbwa na mlipuko wa ugonjwa huo.
Katika hatua nyingine Afisa afya amewasisitiza wazazi na walezi kuhakikisha wanaweka safi mazingira ya nyumbani ili kuwalinda watoto na magonjwa ya kuhara ambapo kwa kipindi cha mwezi July-octoba 2023 watoto 1360 waliugua ugonjwa wa kuhara na watano kati ya hao walifariki.