Viongozi wa dini wakemea ramli chonganishi Kigoma
5 February 2024, 15:32
Jamii imeshauriwa kutojihusisha na vitendo vya ramli chonganishi ambavyo vinafanywa na waganga wa kienyeji ili kuwatapeli wananchi.
Na, Josephine Kiravu
Viongozi wa dini Kutoka madhehebu mbalimbali Mkoani kigoma wamekemea vikali vitendo vinavyoendelea kufanywa na waganga wanaopiga ramli chonganishi maarufu kwa jina la kamchape huku wakiwaonya pia waumini wao kutojihusisha kwa namna yoyote na watu hao.
Askofu wa kanisa la Anglikan Dayosisi ya Kibondo ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCT mkoa wa Kigoma ameeleza hayo kwenye mkutano na wanahabari katika eneo la ukumbi mdogo wa ofisi ya mkuu wa Mkoa wa kigoma ambapo Maaskofu kutoka maeneo mbalimbali wamekutana hapo kwa ajili ya kujadili namna ya kutokomeza ramli chonganishi.
Ameongeza kuwa ni marufuku kwa waumini kuambatana na wapiga ramli chonganishi lakini pia ni maraufuku kwa watu hao kusogelea nyumba za ibada na hata nyumba za viongozi wa dini kwa lengo la kupiga ramli chonganishi na kwamba ni wakati sasa wakufanya maendeleo ya mkoa na si vinginevyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Kigoma Kamishna Jenerali mstaafu wa jeshi la zimamoto na uokoaji Thobias Andengenye amesema mpaka sasa watu kadhaa wamefikishwa mahakamani kwa ajili ya hatua zingine ili iwe fundisho kwa wale wanaoendelea kufanya vitendo hivyo.
Ni takribani mwaka mmoja sasa tangu wimbi la watu wanaojihusisha na upigaji ramli chonganishi kuingia mkoani Kigoma wakianzia kijiji cha Sunuka Halmashauri ya wilaya ya Uvinza na sasa wanatajwa kuonekana kwenye maeneo mengi ya mkoa huu na kuifanya jamii kuwaamini licha ya elimu inayotolewa ikionesha kuwa watu hao ni matapeli.