Halmashauri ya wilaya Kasulu yakusanya zaidi ya bilioni 19
22 January 2024, 09:49
Madiwani wilayani Kasulu Mkoani Kigoma wametakiwa kuendelea kusimamia na kuibua vyanzo vya mapato ili kusaidia kuongeza mapato ya halmashauri hiyo.
Na Hagai Ruyagila – Kasulu
Halmashauri ya wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma imekusanya zaidi ya shillingi billion 19 ambayo ni sawa na asilimia 61 kutoka ruzuku ya serikali, wahisani na vyanzo vya ndani vya mapato vya halmashauri hiyo katika kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba mwaka 2023
Afisa Mipango wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Bw. Fadhili Juma akitoa taarifa ya ukusanyaji mapato kwa kipindi cha nusu ya mwaka wa bajeti 2023/ 2024 amesema halmashauri imekisia kukusanya na kutumia kiasi cha zaidi ya shillingi billion 31 kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato kwa mwaka mzima wa bajeti.
Fadhili amesema katika utekelezaji wa bajeti hiyo halmashauri imehamisha kiasi cha zaidi ya shillingi million 146 kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo kwenye vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu na kwamba utaratibu wa utoaji mikopo ukikamilika fedha hizo zitakopeshwa kwa vikundi husika
Kwa upande wake afisa maendeleo ya jamii halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Bi.Victoria Moses amesema mikopo hiyo inatolewa katika makundi hayo ili kusaidia kuongeza kipato katika familia, jamii na mtu mmoja mmoja na kwamba kwa vikundi vitakavyo pata mkopo huo wajitahidi kurejesha kwa wakati ili kutoa wigo kwa watu wengine kukopeshwa.