madarasa 38 shule za sekondari yakamilishwa wilayani kakonko
9 January 2024, 17:39
Serikali wilayani Kakonko mkoani Kigoma imekamilisha ujenzi wa vyumba 38 vya madarasa katika shule za sekondari wilayani humo hatua itakayowezesha wanafunzi wote waliochaguliwa kidato cha kwanza kuanza masomo kwa wakati
Ujenzi huo uliogharimu shilingi milioni 760 umeambatana na utengenezwaji wa viti na meza kulingana na idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza mwaka huu wa 2024
Mkuu wa wilaya ya Kakonko kanali Evance Malasa wakati wa ukaguzi wa mwisho katika shughuli hiyo ya ujenzi amesema kuwa imekamilika kwa asilimia 90 ambapo pia amewataka maafisa elimu kata kuhakikisha wanafunzi wote waliochaghuliwa wanaanza masomo mara moja.
Baadhi ya wananchi wilayani Kakonko wamepongeza serikali kwa mikakati ya kufanikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa wakati hali ambayo itasaidia kuboresha elimu kote nchini ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo wazazi walikuwa wakilazimika kuchangia gharama za ujenzi licha ya hali duni ya maisha.
Jumla ya wanafunzi 3194 katika halmashauri ya wilaya ya Kakonko mkoani kigoma wamechaghuliwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza kwa mwaka 2024 ambapo serikali imehakikisha miundo mbinu inakamilika kwa wakati na kuondoa changamoto za kuchelewa kuanza masomo na hivyo kuimalisha dhana ya elimu bora kwa wote.