Ndejembi aagiza kuchukuliwa hatua za kinidhamu wahusika wa mradi Kigoma
8 January 2024, 17:15
Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Deogratius Ndejembi amemuagiza Afisa Elimu Sekondari Mkoa wa Kigoma na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kutoa maelezo ya maandishi kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Adolf Nduguru ya kwanini walitoa taarifa ya kukamilika kwa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Nkungwe ilihali ikiwa bado haijakamilika.
Mhe Ndejembi ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa shule za sekondari katika Wilaya ya Kigoma ambapo ameeleza kutoridhishwa na ujenzi wa shule hiyo huku akimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri kumchukulia pia hatua za kinidhamu Mhandisi wa halmashauri na mhandisi anaesimamia mradi huo.
Amesema wamekagua ujenzi wote na kuona kwamba madarasa yenyewe bado hayajakamilika, milango haijafungwa, madawati hayajawekwa na hata vyoli bado halijakamilika huku akisema kuwa kwa uzembe huo hawawezi kukaa kimya lazima hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa wote waliohusika.
Amesema Ofisi ya Rais-TAMISEMI haitomvumilia mtu yeyote atakayejarihu kurudisha nyuma jitihada za Mhe.Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye amepeleka zaidi ya Sh. Milioni 600 kwa ajili ya kumaliza changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu.