Viongozi wa kata, vijiji watakiwa kujadili vipaumbele na wananchi Buhigwe
5 January 2024, 09:39
Viongozi wa vijiji na kata wilayani Buhigwe mkoani Kigoma wametakiwa kuitisha mikutano na wananchi ili kujadili vipaumbele vya miradi ya maendeleo inayotakiwa kujengwa katika maeneo yao.
Na, Michael Mpunije
Wito huo umetolewa na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Buhigwe Bw.Venance Kigwinya wakati akizungumza na radio Joy kuhusu mpango wa ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Chagwe kata ya Mubanga wilayani humo.
Bw. Kigwinya amesema wananchi wanatakiwa kujitolea angalau asilimia 25 ya ujenzi wa zahanati mpaka hatua ya boma ili halmashauri ya wilaya iweze kuomba fedha kutoka serikali kuu kwa ajili kukamilisha ujenzi huo kulingana na mahitaji ya wananchi.
Aidha kigwinya ameongeza kuwa bado vipo baadhi ya vijiji ambavyo havina zahanati katika wilaya hiyo, hivyo wananchi, viongozi wa vijiji na kata wanatakiwa kuweka vipaumbele vyao juu ya miradi ya maendeleo pamoja na ujenzi wa huduma za jamii zinazotakiwa kujengwa katika maeneo yao.