Polisi kushirikiana na wasaidizi wa kisheria Kibondo
4 January 2024, 15:40
Mkuu wa wilaya ya Kibondo mkoani kigoma Kanali Agrey Magwaza amelitaka Jeshi la Polisi wilayani Humo kwa kushirikiana na wasaidizi wa Kisheria , kutoa elimu kwa wananchi kuhusu Haki ya Mtuhumiwa anapokamatwa ili kuondoa mkanganyiko na mitazamo waliyonayo wananchi juu ya jeshi la polisi katika zoezi la ukamataji wahalifu.
Amesema hayo katika Hafla Fupi ya Kukabidhi Vyeti kwa wasaidizi wa kisheria 11 wa shirika la Kibondo paralegal Foundation KIPAFO ili kuwatambua na kutambua mchango wao kwa wilaya ya kibondo katika kuelimisha wananchi juu ya masuala ya sheria.
Aidha kanali Magwaza amesema kuwa asilimia kubwa ya wananchi wamekuwa hawajui haki zao na wakati mwingine kushindwa kutoa ushirikiano wa kutosha hali ambayo husababisha kesi kuwa ngumu na hivyo kufanya shughuli za upelelezi wa kesi mbali mbali kuwa ngumu
Mkuu wa jeshi la Polisi wilaya ya Kibondo Mrakibu wa polisi Philibert Omrushaka amepongeza jitihada za wasaidiza wa kisheria wilayani humo kwa kuwa elimu wanayoitoa inasaidia kupunguza makosa ya jinai yanayofanywa na wananchi.
Awali mratibu wa miradi wa shirika la Kibondo Paralegal Foundation Bw. Hafidhi Ramadhani amesema pamoja na kutoa elimu kwa wananchi wamewajengea uwezo viongozi wa jamii ili kuimarisha upatikanaji wa haki katika majukumu wanayoyasimamia kwenye maeneo yao.