Wazazi kuchukuliwa hatua kwa kushindwa kumpeleka mtoto shule Kasulu
4 January 2024, 15:02
Wazazi na walezi wilayani Kasulu Mkoani Kigoma wametakiwa kuwapelekea watoto wao shule ili waweze kupata elimu itakayo wasaidia katika maisha yao ya kila siku.
Akizungumza na vyombo vya habari mjini Kasulu Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi wilayani Kasulu Selemani Malumbo amesema endapo mzazi au mlezi hata mpeleka mtoto wake shule wakati tayari umri wake unafaa kuandikishwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Aidha Malumbo amesema tayari baadhi ya wazazi wamekuwa na mwitikio mzuri wa kuwaandikisha watoto wao ili waanze masomo yao ya awali hivyo wanatakiwa kuhimizwa na kufuatilia maendeleo ya mtoto wake ili atimize ndoto zake.
Kwa upande wao wazazi na walezi wamesema hilo ni jukumu lao na tayari wameshatimiza wajibu wao wa kuwaandikisha watoto wao ili wapate elimu itakayowasaidia katika maisha yao.
Pia wamesema suala la kukagua maendeleo ya watoto wao shuleni ili kujuwa walichojifunza wanaofanya hivyo ni wachache kutokana na wazazi wengi kuwa wakulima jambo linalopelekea mzazi kujikita kwenye kilimo zaidi.