Mashirika, wananchi watakiwa kuwakumbuka watoto yatima Kigoma
3 January 2024, 12:30
Wito umetolewa kwa mashirika na wananchi wa mkoani Kigoma kujitokeza na kuchangia vitu mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia watoto wanaolelewa na kituo cha malezi ya watoto Matyazo.
Na Lucas Hoha
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Joy in the Harvest na Radio Joy Mwenge Muyombi, mara baada ya shirika hilo kutoa msaada wa vitu mbalimbali katika kituo hicho ili kuwatia moyo watumishi wa kituo hicho na watoto ili wajione kuwa sehemu ya jamii.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Afisa ustawi wa jamii wa Halmashauri hiyo Exavery Joseph ameshukuru uongozi wa Shirika la joy kutoa msaada huo kwani wameunga mkono serikali katika kuwahudumia watoto wanaotoka kwenye mazingra magumu wakiwemo waliotelekezwa na wazazi.
Kwa upande wao, Baadhi ya watumishi wanaolea watoto hao akiwemo Katibu wa afya wa kituo hicho Jangwe Anania na mwangalizi wa watoto hao Petrovia Damiano, wamesema licha ya wadau kujitolea kuwasaidia bado wanamahitaji ya vitu mbalimbali, huku wakiomba wadau hao kuendelea kuwaunga mkono.