wananchi Kigoma walalamikia TARURA kuelekeza maji ya mitaro mingi kwenye makazi ya watu
18 December 2023, 13:55
Wananchi wa Mtaa wa Katubuka maeneo ya Bwawani Kata ya Katubuka Manispaa ya Kigoma Ujiji wamelalamikia Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini TARURA kuelekeza mitaro mingi ya maji kwenye mtaa huo na kupelekea mtaa huo kujaa maji kipindi cha masika na kuleta athari ikiwemo nyumba kuanguka.
Na, Lucas Hoha
Wananchi hao wametoa malalamiko hayo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Salum Kalli alipotembelea maeneo hayo kwa lengo lakutoa tahadhari kwa wananchi wanaokaa eneo hilo ambalo limekuwa likijaa maji hasa mvua zinaponyesha
Wananchi hao wamesema miaka kadhaa iliyopita maji yalikuwa yamepungua lakini baada ya mitaro mingi inayosafirisha maji kuelekezwa mtaa huo umesababisha maji kuwa mengi na wengine wamehama makazi yao.
Mara baada ya Malalamiko hayo Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Salum Kalli, hapa anatoa maelekezo kwa wakala wa barabara za Mjini na Vijijini TARURA na wataalamu wengine wa Manispaa kufanya tathimini ya namna ya kuboresha miundombinu katika maeneo hayo ili kuwanusuru wananchi.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Meneja wa Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini TARURA Mhandisi Felician Kavishe amesema wanaenda kuandaa bajeti ili kuboresha miundombinu ya maeneo hayo kwa ajili ya usalama wa wananchi.
Aidha Mkuu wa Wilaya Salum Kalli ametoa wiki moja kwa watu wanaofuga mifugo katika maeneo hayo kuondoa mifugo hiyo huku amesimamisha ukumbi wa starehe uliopo eneo hilo kuacha kuendesha shughuli zake na kusitisha baadhi ya viwanda vidogo vinavyotumika kuchakata mafuta ya mawese katika eneo hilo.