Milioni 430 zaondoa kero ya maji kata ya Businde Kigoma
15 December 2023, 10:07
Wakazi wa kata ya Businde Manispaa ya Kigoma Ujiji wameondokana na adha ya ukosefu wa maji safi na salama baada ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa mazingira (KUWASA) kukamilisha mradi wa bomba la maji lenye urefu wa kilometa tano linalopeleka maji katika kata hiyo.
Kata ya Businde ni moja kati ya maeneo ambayo kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la watu ambapo changamoto kubwa kwa wakazi wa kata hiyo ilikuwa ni huduma ya maji na wakazi wake walilazimika kununua huduma hiyo muhimu kwa gaharama kubwa au kuifuata mbali na makazi yao lakini kwa sasa adha hiyo imefika mwisho.
Mhandisi wa Mtandao wa Maji kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Manispaa ya Kigoma Ujiji, KUWASA, Francis Makoye, amethibitisha kuwa kwa sasa huduma ya maji katika kata ya Businde inapatikana muda wote baada ya kazi ya takribani miezi mitatu ya kuunganisha bomba kutoka katika kata ya Kagera.
Hata hivyo Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Kigoma, ikiongozwa na mwenyekiti wake Ahmed Mwilima imefika katika kata ya Businde kukagua utekelezaji wa miradi mbali mbali na kueleza kuridhishwa na mradi huo.
Mradi wa kupeleka bomba la maji Businde ni sehemu ya mradi mkubwa wa kuongeza mtandao wa maji kwa kilometa 90 katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Manispaa ya Kigoma Ujiji, KUWASA kwa gharama ya Shilingi Bilioni 1.9.