Uchumi wa wavuvi Kigoma kuchochewa na vifaa vya kisasa walivyokabidhiwa
20 November 2023, 13:55
Baadhi ya wavuvi wanaofanya shughuli za uvuvi ndani ya Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma wanatarajia kujikwamua kiuchumi baada ya serikali kuwawezesha zana za kisasa za uvuvi ikiwemo boti 9 na vifaa vyake zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 500.
Na, Lucas Hoha
Wakizungumza na kituo hiki mara baada ya kupatiwa zana hizo baadhi ya wavuvi hao wamesema kupata vifaa hivyo watafanya kazi yenye tija tofauti na zamani walipokuwa wanatumia zana zilizopitwa na wakati na kuwafanya kupata mazao madogo ya samaki
Awali akikabidhi zana hizo, Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi Alexander Pastory Mnyeti amesema Serikali imejipanga kuwawezesha wananchi katika makundi tofauti huku akitoa wito kwa Maafisa Uvuvi kuacha tabia ya kuwachonganisha wananchi na Serikali bali wajikite kutoa Elimu kuhusu Uvuvi haramu.
Kwa Upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya mifugo na Uvuvi, Tanzania Agnes Meena amesema zana hizo za Uvuvi wanazitoa kwa kushirikiana na Benki ya maendeleo ya Kilimo Tanzania na mpaka Jumla ya boti 160 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 11.5 zitatolewa kwa awamu ya kwanza kwa wavuvi nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Kanali Michael Ngayalina amesema Serikali imeendelea kuboresha miundombinu katika Mkoa wa Kigoma katika sekta ya Barabara, Elimu, maji Uvuvi na kilimo na kuwa Mkoa huu utakuwa ni lango la kufanyia biashara na kukuza uchumi wa nchi za Congo na Burundi.