Watu wasiojulikana wavunja vibanda 13 vya biashara manispaa ya Kigoma
3 November 2023, 16:39
Kubomolewa kwa vibanda hivyo kunatajwa kuwarudisha nyuma wafanyabiashara wakubwa na wadogo kwani ndio sehemu pekee walitegeme kujipatia kipato.
Na Emmanuel Matinde
Watu wasiojulikana wanaokisiwa idadi yao kuwa ishirini wamevunja kuta za vibanda vya biashara 13 kati ya 25 vinavyojengwa katika eneo la stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani iiyoko Masanga mjini Kigoma na kusababisha hasara ya takribani Shilingi Milioni 90.
Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji ilitangaza zabuni ya uwekezaji katika kujenga vibanda vya biashara ambapo wafanyabiashara Ulimwengu Rashid Malima na mwenzake Shabani Yasini Nyaburura, walishinda zabuni hiyo na mwezi Februari mwaka jana walianza ujenzi wa vibanda hivyo.
Hata hivyo katika hali isiyo ya kawaida kila inapofikia hatua ya kukamilika hubomolewa na tukio la hivi karibuni kabisa ni Oktoba 30, na hivyo kuathiri wafanyabiashara zaidi ya ishirini waliowekeza katika jengo hilo.
Kufuatia matukio hayo ambayo hufanywa nyakati za usiku, mmoja katika wamiliki wa vibanda hivyo Ulimwengu Rashid Malima, amevishutumu vyombo vya dola ngazi ya wilaya kwa kushindwa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya hujuma hizo na kuomba ngazi za juu za serikali kuingilia kati jambo hilo.
Hata hivyo Baadhi ya mawakala wa tiketi za mabasi pamoja na baadhi ya wafanyabiashara ndogo ndogo katika eneo la stendi kuu ya mabasi Masanga, ambao wanatarajia kunufaika na uwekezaji huo wamelaani vikali kitendo hicho kuwa ni cha kinyama.
Suala hilo limetinga katika Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, huku kukiwa na sintofahamu juu ya mchakato wa uwekezaji kama ulifuata njia sahihi. Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Salum Kalli, ameelekeza awali ya yote hatua zichukuliwe dhidi ya anayehusika na hujuma hiyo.