Serikali kuendelea kutatua changamoto za wafanyabiashara Kigoma
1 November 2023, 15:32
Wafanyabiashara wameomba serikali kuweka mazingira rafiki ili waweze kufanya vizuri katika kufanya baishara ndani na nje ya nchi.
Na Lucas Hoha
Serikali imewahakikishia wafanyabiashara wa mkoa wa Kigoma kuwa inaendelea kutatua changamoto na vikwazo vinavyowafanya kushindwa kufanya biashara ikiwemo kuboresha miundombinu ya usafirishaji, kuondoa vikwazo mipakani ili kuinua uchumi wa mkoa wa Kigoma
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Thobias Andengenye wakati akifungua kikao cha baraza la wafanyabiashara mkoa wa Kigoma ambapo amesema serikali inaendelea kutekeleza mikakati hiyo ili kuongeza fursa kwa wafanyabiashara kujiandaa katika uwekezaji.
Kwa upande wao baadhi ya wafanyabiashara wamesema kuna kila sababu ya serikali kukamilisha miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa soko la Mwanga na kufungua bandari kavu ya Katosho ili kuweka urahisi wa kufanya biashara na nchi jirani ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Akitoa ufafanuzi kuhusu ujenzi wa soko la Mwanga, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji Mwantum Mgonja amesema hatua iliyopo kwa sasa wanaendelea na manunuzi ya vifaa na kumtafuta mkandarasi na kuwa ifikapo mwakani mwezi Februari ujenzi utaanza.
Masuala mengine yaliyojadiliwa katika kikao hicho ni kuweka ujirani mwema kati ya Kigoma na DRC, kurahisisha upatikanaji wa vitamburisho vya taifa NIDA na kuondoa baadhi ya tozo katika bandari za Kigoma ili kuwavutia wafanyabiashara.