Wafanyabiashara Kigoma watakiwa kufuata kanuni na sheria za BoT
20 October 2023, 15:41
Wafanyabiashara mkoani Kigoma wametakiwa kufuata sheria za kubadilisha fedha za kigeni ili kuepuka kuingia kwenye migogoro na kuhujumu uchumi.
Na, Lucas Hoha.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Kigoma ACP Filemon Makungu amewataka wafanyabiashara wanaofanya biashara ya kubadilishana fedha za kigeni kufuata kanuni na sheria zinazotolewa na Benki kuu ya Tanzania ili kuepuka adhabu ikiwemo kufunguliwa mashtaka ya uhujumu uchumi.
Makungu ametoa wito huo wakati Semina iliyowakutanisha baadhi ya viongozi kutoka Benki kuu ya Tanzania, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma na wafanyabiashara iliyolenga kuwajengea uelewa juu ya kanuni mpya za biashara ya kubadilishana fedha za kigeni ya Mwaka 2023.
Naye Afisa kutoka Benki kuu ya Tanzania kitengo cha masuala ya biashara ya kubadilishana fedha Omary Msuya amesema baada ya kanuni hizo mpya mtu hataruhusiwa kufanya biashara ya kubadilishana fedha bila ya kusajiliwa na benki kuu, huku akiwataka wananchi kuacha kuamini biashara za kubadilishana fedha zinazofanyika kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa upande wao baadhi ya wafanyabiashara mkoa wa Kigoma wameomba serikali kuweka mazingira rafiki kwa wananchi juu ya namna ya kufungua maduka ya kubadilishana fedha za kigeni ili kujikwamua kiuchumi na kuongeza uchumi wa mkoa wa Kigoma.