Zaidi ya watu 40 wanashikiliwa na Polisi Kigoma kwa kuhusika kwenye vurugu
11 October 2023, 09:11
Jeshi la Polisi Mkoani Kigoma limewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa za vitendo vya wizi na uhalifu kwenye maeneo yao.
Na, Josephine Kiravu.
Zaidi ya watu 40 wanashikiliwa na Jeshi la polisi Mkoani Kigoma kwa tuhuma za kuhusika kwenye vurugu zilizotokea hivi karibuni katika eneo la Kazuramimba Halmashauri ya wilaya ya Uvinza na kusababisha vifo vya watu 3.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Kigoma ACP Philemon Makungu amethibitisha kukamatwa kwa watu hao na kwamba taratibu zingine zinaendelea kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
Kamanda Makungu ameongeza kuwa Jeshi la polisi halitofumbia macho watu ama kundi ambalo linachochea uvunjifu wa amani na kwamba wataendelea kuwachukulia hatua stahiki watakaobainika kuvunja sheria.
Katika hatua nyingine Kamanda makungu ameeleza mafanikio katika operesheni zilizofanyika hivi karibuni na kufanikiwa kukamata silaha moja aina ya pisto CZ83 Browing yenye namba TZCAR950117 ikiwa na magazine 02 pamoja na pikipiki 3 ambazo zimekuwa zikitumika kwenye matukio ya uhalifu ikiwemo uporaji mikoba.
Jeshi la polisi limewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuzuia na kubaini wahalifu kwa lengo la kuimarisha usalama wa raia na mali zao.