Shule ya msingi Busunzu B yakabiliwa na uhaba wa madawati 400
26 September 2023, 12:21
Benki ya NMB kanda ya magharibi imetoa msaada wa madawati 50 katika shule ya msingi Busunzu Biliyopo Wilayani kibondo Mkoani Kigoma ikiwa ni jitihada za kukabiliana na uhaba wa madawati katika shule hiyo.
Na James Jovin
Shule ya msingi Busunzu B, iliyoko wilayani Kibondo mkoa wa Kigoma inakabiliwa na uhaba wa madawati zaidi ya 400 hali inayosababisha changamoto kwa wanafunzi wengi kukalia dawati moja hivyo kushindwa kujisomea kwa uhuru.
Miongoni mwa wanafunzi waliozungumza na Radio Joy Fm wamesema kuwa hali hiyo imekuwa ikisababisha kushuka kitaaluma kwa kuwa hawawezi kusoma kama ilivyo kwa wanafunzi wengine na wakati mwingine kulazimika kuandikia chini.
Kwa upande wake, mkuu wa shule ya msingi Busunzu B, mwalimu Felix Fredrick amesema kuwa shule ya msingi Busunzu B. ina jumla ya wanafunzi 2,957 hivyo idadi hiyo ni kubwa ukilinganisha na madawati yaliyopo na kupelekea zaidi ya wanafunzi watano kukalia dawati moja.
Kutokana na changamoto hiyo Benki ya NMB Kanda ya Magharibi imejitolea madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni 5 ikiwa ni sehemu ya kurudisha shukrani kwa jamii lakini pia kusaidia kupunguza tatizo hilo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Magharibi Bw. Nseka Urio amesema kuwa benki hiyo imekuwa ikitoa misaada mbalimbali hasa katika sekta ya elimu, afya na majanga mbalimbali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma Kanali Agrey Magwaza ambaye alikuwa mgeni rasmi katika shughuli hiyo amewataka wanafunzi kusoma kwa bidii ili kupiga vita maadui watatu ambao ni ujinga, umasikini na maradhi.