DC Kasulu awataka vijana wa JKT Mtabila kuwa wazalendo
11 September 2023, 13:21
Vijana waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa JKT Kambi ya Mtabila Wialayni Kasulu Mkoani Kigoma wametakiwa kuwa wazalendo.
Na Hagai Ruyagila
Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanal Isack Mwakisyu amewataka wahitimu wa mafunzo ya awali ya kijeshi kikosi namba 825 Mtabila JKT kwenda kuyatekeleza kwa vitendo katika jamii yote waliyojifunza kwa kipindi chote cha mafunzo.
Kanal Mwakisyu ameyasema hayo wakati akizungumza na wahitimu wa mafunzo ya vijana wa mujibu wa sheria operation miaka 60 ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambao wamepata mafunzo ya kijeshi kwa kipindi cha majuma 12.
Aidha Kanal Mwakisyu amesema mafunzo ya JKT huwaandaa vijana kuwa wazalendo na wenye nia ya kulijenga taifa lao kwa upendo popote watakapotumwa.
Kwa upande wake kamanda kikosi namba 825 Mtabila JKT Luteni Kanal Patrick Ndwenya amewataka vijana waliohitimu pindi watakapokuwa majumbani kwao kuepuka kujiingiza katika vikundi viovu vya matumizi ya madawa ya kulevya, wizi na ulevi na badala yake waendeleze tabia njema ambayo wamefundishwa kwa kipindi chote walichokuwa kambini.
Nao baadhi ya wahitimu wa mafunzo ya awali ya kijeshi kikosi namba 825 Mtabila JKT wamaesema mafunzo hayo yamewasaidia kwa kiasi kikubwa pindi watakaporudi nyumbani.