Wakuu wa wilaya, wakurugenzi kusimamia mpango wa usajili wa watoto
6 September 2023, 16:03
Viongozi wa Halmashauri Mkoani Kigoma wametakiwa kuhakikisha watoto wanasajiliwa.
Na, Josephine Kiravu
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Thobias Andengenye amewaagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri zote mkoani hapa kusimamia vyema mpango wa usajili wa watoto walio chini ya miaka 5 ili kuongeza idadi ya watoto wanaosajiliwa kwa mwaka.
Akitoa maagizo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma katika ufunguzi wa Semina kwa viongozi wa wilaya na mkoa pamoja na viongozi wa dini Mkuu wa wilaya ya Buhigwe Kanal Michael Ngayalina amesema ili kurahisisha zoezi hili ambalo litadumu kwa majuma mawili wakurugenzi na wakuu wa wilaya wanapaswa kutoa ushirikiano ili kurahisisha zoezi hilo.
Kwa upande wake, Naibu Kabidhi Wasii Mkuu Bi. Irene Lesulie amesema hali ya usajili wa watoto bado ipo chini kwani kwa mwaka 2022 ni asilimia 10 tu ya watoto waliozaliwa ndio waliofanikiwa kusajiliwa kwenye mfumo.
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi Msaidizi huduma za ustawi wa jamii-TAMISEMI Bi Mariam Nkumbwa amesema miongoni mwa changamoto walizobaini ni pamoja na wahudumu wa afya kuchelewa kuingiza idadi ya watoto wanaozaliwa kwenye mfumo.
Mganga mkuu mkoa wa Kigoma Dr Jesca Leba nae akabainisha mikakati waliyonayo katika kuhakikisha watoto wanaozaliwa wanasajiliwa kwa wakati.
Nao badhi ya viongozi wa dini waliohudhuria katika mafunzo hayo akiwemo Shekhe Haroon Shaarawy na Mchungaji Augustino Kizeba wamesema zoezi hili litasaidia watoto wengi kupata vyeti vya kuzaliwa na kupunguza usumbufu kwa wazazi.
Hata hivyo licha ya uwepo wa changamoto katika ukusanyaji wa taarifa na mlundikano wa wananchi kwenye vituo vya usajili lakini zaidi ya watoto 8,646,324 wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa katika mikoa 24 ambayo imeanza kutekeleza mpango huu.