Vijana waliohitimu mafunzo JKT Bulombora watakiwa kuwa wazalendo
6 September 2023, 12:39
Kikosi cha Jeshi la kujenga Taifa JKT Bulombora kimesema kitaendelea kuwafundisha ujuzi na uzalendo vijana wote ili waweze kulitumikia Taifa.
Na, Tryphone Odace.
Vijana waliohitimu mafunzo ya kijeshi oparesheni miaka 60 katika kambi ya Jeshi la kujenga Taifa JKT, kikosi cha Jeshi 821 KJ Bulombora wametakiwa kuwa wazalendo katika kuilinda Nchi na kuhakikisha wanakuwa sehemu ya kudhibiti vitendo vya uvunjifu wa amani.
Haya yameelezwa na Mwakilishi wa Mkuu wa Jeshi la kujenga Taifa Kanali Peter Lushika wakati wa kufunga mafunzo kwa vijana kwa mujibu wa sheria Operasheni miaka 60 ambapo amesema wanatakiwa kuendelea kuonyesha uzalendo kwa Taifa na kutojihusisha na vitendo viovu kwenye jamii.
Naye Mkuu wa kikosi cha 821 KJ Bulombora Luteni Kanali Juma Hongo amesema mbali na vijana hao kupatiwa mafunzo mbalimbali wamewawezesha kupata stadi za maisha kupitia uzalishaji mali huku, Mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi Brigedia Jenerali Solotina Nshushi akiwataka kujiepusha na vitendo vitakavyohatarisha afya zao.
Awali wahitimu hao kupitia risala yao wamesema kuwa mbali na kupatiwa ujuzi mbalimbali wameeeleza kambi hiyo inakabiliwa na changomoto za uhaba wa maji na umeme wa uhakika.
Akifunga mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya Kigoma Salum Kalli amesema Serikali inaendelea kujivunia vijana hao kwani ni tunu kubwa katika kuhakikisha wanalinda nchi na atahakikisha anashughulikia changamoto hizo.