Wanafunzi walia na ukatili wa kijinsia Kigoma
1 September 2023, 11:16
Katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, Shirika la Maendeleo ya Vijana mkoani Kigoma KIVIDEA limeendelea kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili kuwapa elimu ya kujitambua ili waweze kuepukana na vitendo vya ukatilii.
Na, Tryphone Odace
Wanafunzi katika shule za msingi na sekondari Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma, wameiomba serikali na mashirika ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kusaidia kudhibiti vitendo hivyo vinavyowakumba baadhi ya wanafunzi ili waweze kutimiza ndoto na malengo waliyonayo.
Hayo yameelezwa katika mdahalo ulioandaliwa na Shirika la Maendeleo ya Vijana KIVIDEA mkoa wa Kigoma wakati likitoa elimu ya vitendo vya ukatili kwa wanafunzi na viongozi, kupitia mradi wa Afya Yangu Maendeleo Yangu unaotekelezwa katika shule kumi za manispaa ya Kigoma Ujiji.
Meneja mradi huo kutoka KIVIDEA Jackline Kitema amesema wanaendelea kuelimisha jamii na wanafunzi kuchukua hatua za kidhibiti vitendo vya ukatili.
Amesema kupitia mradi huo wameweza kuwakutanisha wanafunzi mbalimbali kutoka shule tofautitofauti ili kuwapa elimu ya namna ya kujitambua ili waweze kuepekana na ushawishi unaoweza kuwasababishia kuingia kwenye vitendo vinavyoweza kuwadhalilisha.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji kata ya Kitongoni Josephat Rusomyo amesema wamelazimika kuunda kamati ya ulinzi wa mtoto ili kusaidia kuchukua hatua kudhitibi vitendo vya ukatili.
Shirika la Maendeleo ya Vijana Kividea mkoani Kigoma linatekeleza mradi wa ujana wangu maendeleo yangu katika manispaa ya Kigoma Ujiji pamoja na Halmashauri ya wilaya Uvinza ukiwa na lengo la kuwapa ujuzi, elimu ya kujitambua, madhara ya madawa ya kulevya na kupinga vitendo vya unyanyasaji kwa watoto.