Waziri Mbarawa atoa siku 15 kwa mkandarasi Kigoma
31 July 2023, 16:22
Na, Emmanuel Matinde
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa, ametoa siku 15 kwa mkandarasi kampuni ya Sinohydro Corporation inayojenga kipande cha pili cha barabara ya Kabingo – Manyovu mkoani Kigoma kufikisha mitambo eneo la kazi ili kukamilisha ujenzi wa mradi huo kwa wakati.
Kipande hicho cha barabara kuanzia Kanyani mpaka Mvugwe chenye urefu wa kilometa 70.5 kinachojengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 83.7 mpaka sasa kimefikia asilimia 65.30 huku mkandarasi akiwa amebakiza muda wa miezi miwli na nusu kwa mujibu wa mkataba.
Mradi huo ni sehemu ya ujenzi wa barabara ya Kabingo wilayani Kakonko hadi Manyovu wilayani Buhigwe yenye urefu wa jumla ya kilometa 260.1 ambayo kukamilika kwake kutafanya mkoa wa Kigoma kufunguka kimiundombinu na kuunganisha na nchi jirani ya Burundi.
Hata hivyo kasi ya ujenzi kwa baadhi ya wakandarasi ni ndogo ambapo baada ya kutembelea mradi wa barabara hiyo unaojengwa na wakandarasi wanne waziri Prof. Mbarawa akatoa kauli ya serikali.
Aidha wakandarasi wengine watatu utekelezaji wake unakwenda vizuri huku baadhi ya maeneo yakiwa tayari yamewekwa lami hatua ambayo wananchi wameanza kuifurahia.
Katika hatua nyingine Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa, amewataka Wakala wa Barabara nchini TANROADS kutembelea miradi inayotekelezwa ili kubaini changamoto na kuzitatua ili mradi huo usonge mbele haraka.
Mradi wa barabara ya Kabingo – Manyovu yenye urefu wa kilometa 260.1 unaojegwa unagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 360.5 na kulingana na mkataba unatakiwa kukamilika mwaka huu kwa vipande vyote vinne.