Serikali yatakiwa kumsimamia mkandarasi bandari ziwa Tanganyika
31 July 2023, 15:32
Serikali imetakiwa kumsimamia mkandarasi anayejenga mradi wa bandari ya ziwa Tanganyika ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa.
Na, Tryphone Odace
Wananchi mkoani Kigoma pamoja na wafanyabiashara wanaosafirisha bidhaa katika nchi jirani, wameiomba serikali kumsimamia mkandarasi anayejenga miradi ya bandari katika ziwa Tanganyika ili ikamilike kwa wakati na kuchochea ukuaji wa kibiashara na uhusiano na nchi jirani.
Wamesema hayo wakati wa ziara ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa, alipotembelea na kukagua ujenzi wa gati za bandari za Kibirizi na Ujiji zilizopo mkoani Kigoma.
Akieleza mwenendo wa ujenzi wa mradi wa bandari za ziwa Tanganyika msimamizi wa mradi, mhandisi Eli Mtaki amesema mradi umechelewa kukamilika kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, licha ya baadhi ya gati kukamilika kwa asilimia mia moja.
Aidha Waziri Mbarawa ameagiza miradi ya bandari kukamilika kwa wakati ili kuleta ufanisi wa kibiashara hasa unaolenga kuinua uchumi wa watanzania na taifa.