Mtoto aliyechomwa moto mikoni kwa kuiba muwa apata matibabu
27 July 2023, 10:58
Kufuatia mtoto wa miaka mitano kuchomwa moto mikono na mama yake mzazi Esther Damiani mnamo tarehe Juni 29 mwaka huu baada ya kuiba muwa, hatimaye mtoto huyo anaendelea vizuri kutokana na matibabu anayoendelea kupatiwa.
Na, Hagai Ruyagila.
Akizungumza na Radio Joy FM, Zuhura Kassimu Kasheshe Katibu wa Dawati la jinsia kata ya Mwandiga amesema maendeleo ya mtoto huyo yanatia moyo kutokana na matibabu anayoendelea nayo.
Bi. Zuhura Kasheshe amewasihi wazazi na walezi wa kata hiyo kudhibiti hasira wanazokuwa nazo baada ya watoto kufanya vitendo ambavyo haviwapendezi ili kutosababisha madhara ndani ya familia na katika jamii inayowazunguka.
Hata hivyo Radio Joy FM imezungumza na Tito Mahamudu Kilalika mwenyekiti wa dawati la jinsia kata ya Mwandiga na mwenyekiti wa kitongoji cha Uwanjani ili kujua kama elimu ya ukatili inatolewa kufuatia matukio hayo ya ukatili kujirudia mara kwa mara.
Kwa upande wake mama mzazi wa mtoto huyo Esther Damiani aliyemfanyia ukatili huo mtoto wake amesema, hatorudia kufanya ukatili wa aina yoyote na kwa mtu yeyote kutokana na madhira ambayo ameyaona mtoto wake akipitia kipindi akipatiwa matibabu.
Ni takribani siku ishirini na nane zimepita tangu mtoto huyo alipofanyiwa ukatili wa kinjinsia na mama yake mzazi baada ya kuiba muwa wenye thamani ya shilingi 200/= katika mtaa wa Uwanjani ndani ya kata hiyo.