Kigoma: Wananchi watakiwa kuacha shughuli karibu na hifadhi za barabara
21 July 2023, 12:02
Wananchi Mkoani Kigoma wametakiwa kuacha kufanya shughuli za kibinadamu katika ya hifadhi za barabara
Na, Josephine Kiravu
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Jenerali Mstaafu wa jeshi la zimamoto na uokoaji Thobias Andengenye amewataka wakazi wa Mkoani hapa kufuata sheria na kuacha kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo ya hifadhi za barabara.
Andengenye ametoa maelekezo hayo wakati akifungua kikao cha bodi ya barabara kwa Mkoa wa Kigoma ambapo amewaelekeza pia wakuu wa wilaya kusimamia ipasavyo na kamwe wasiruhusu wajasiriamali kufanya shughuli zao kwenye hifadhi za barabara.
Ameongeza kuwa kuendelea kuwaacha wananchi kuishi na kufanya shughuli mbalimbali kwenye hifadhi za barabara kunachangia kusababisha fidia na madai yasiyokuwa ya lazima kwa Serikali pale wanapotakiwa kupisha maeneo hayo.
Kwa upande wake Meneja wa TANROADS mkoa wa Kigoma Mhandisi Narcis Choma amesema tatizo la uvamizi wa barabara sio kwa mjini pekee hata vijijini uvamizi wa barabara bado unaendelea kufanyika licha ya elimu inayoendelea kutolewa kwa jamii.
Katika hatua nyingine Mbunge wa jimbo la Kigoma Mjini Kirumbe Ng’enda amezitaka Halmashauri Mkoani hapa kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwenye fedha zinazotokana na mapato ya ndani ili kupunguza mzigo kwa TARURA.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa ameitaka TANROADS na TARURA mkoani Kigoma kuongeza kasi kwenye ujenzi wa barabara pamoja na kuwachukulia hatua wakandarasi wazembe watakaoshindwa kukamilisha miradi kwa wakati ama kwenye ubora uliokusudiwa.