Vijiji 8 Kigoma vyakabiliwa na ukosefu wa maji
13 July 2023, 11:58
Ukosefu wa maji katika baadhi ya vijiji vya halmashauri ya wilaya na mkoani Kigoma umetajwa kuendelea kuwatesa wananchi kwani hulazimika kutumia maji ya visima na mito yasiyokuwa safi na salama.
Na, Kadislaus Ezekiel
Wananchi wa vijiji vinane vya halmashauri ya wilaya ya Kigoma mkoani Kigoma wanalazimika kutumia maji ya mito, chemichemi na visima kwa kukosa huduma ya maji safi na salama huku baadhi wakikumbwa na magonjwa ya minyoo na kuhara.
Baadhi ya wenyeviti wa vijiji wakizungumza wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa tathmini ya upatikanaji wa maji kwa wilaya ya Kigoma, wameiomba serikali kukamilisha miradi inayojengwa ili kuondokana na adha ya kukosa maji safi na salama.
Meneja wa wakala wa usambazaji maji na usafi wa mazingira vijijini RUWASA wilaya ya Kigoma mhandisi Leo Respisius Mwombeki amesema wanaendelea kuchukua hatua za kukamilisha miradi inayotekelezwa na kufikia vijiji vyote katika bajeti ya mwaka huu.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kigoma Salum Kalli amemwagiza meneja wa Ruwasa kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati ili iweze kutoa huduma kwa wananchi wote.