DC kigoma amepiga maarufuku ramli chonganishi kwenye jamii
11 July 2023, 10:54
Serikali imesema itawachukulia hatua za kisheria yeyote atakaye jihusisha ama kusaidia shughuli za Rambaramba (Kamchape) wanaopiga ramli chonganishi na haitawaonea huruma.
Na, Lucas Hoha
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Salum Kalli ameomba viongozi wa Dini pamoja viongozi wa Serikali za mitaa kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama kukemea vitendo vya ramli chonganishi zinazofanywa na waganga wanaojiita Kamchape kwani vinasababisha uvunjifu wa amani kwenye jamii.
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Radio Joy fm, ambapo amekea vikali ramli chonganishi ndani ya Wilaya hiyo na kuongeza kuwa mtu atakayebainika anaunga mkono kitendo hicho atakamatwa na kufunguliwa mashitaka .
Aidha Mh. Kalli amesema uongozi wake hautaruhusu mkutano wowote unajadili masuala ya ramli chonganishi, huku akiomba wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya ramli chonganishi.
Kwa upande wao wananchi wa kata ya Bitale Halmashauri ya Wilaya Kigoma licha ya kuamriwa na Mkuu wa Wilaya kusitisha mpango huo haramu, wameashiria kushikilia msiamamo wao wa kuendelea kushirikiana na waganga wapiga ramli ili kuondoa ushirikina.
Hata hivyo Diwani wa Kata ya Bitale Albogast Paul Ndiyunze, ameeleza waganga wapiga ramli hao wanaingia katika maeneo yao kwa kupata ushirikiano kutoka kwa baadhi ya wananchi na kuwa viongozi wa serikali za mitaa wataendelea kuhakikisha wanatoa taarifa za wanaohamasisha ramli chonganishi.
Kamchape ni kikundi cha waganga wapiga ramli chonganishi maarufu lambalamba wanajihusisha na kupiga ramli ilikuwwabaini wanaofanya vitendo vya ushirikina kwenye jamii.