Wahitimu Kigoma watakiwa kufundisha maadili mema kwenye jamii
10 July 2023, 11:56
Suala la maadili kwenye jamii limeendelea kuwa changamoto ambapo wahitimu wa vyuo mbalimbali wametakiwa kuwa mfano kwa jamii na kuhimiza maadili ili kuwa na kizazi chenye maadili mazuri.
Na Lucas Hoha.
Wito umetolewa kwa wanafunzi wanaomaliza masomo katika kada mbalimbali kuwa mstari wa mbele katika kuwatetea wananchi na kuifundisha jamii kuwa na maadili mema.
Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki Kigoma, Joseph Mlola amesema hayo wakati wa mahafali ya 22 ya chuo cha Kigoma Training College KTC kilichopo manispaa ya Kigoma Ujiji, ambapo ameeleza kuwa baadhi ya wasomi wamekuwa hawakemei vitendo viovu hali ambayo imepelekea kuwepo kwa mmomonyoko wa maadili.
Kwa upande wake mkuu wa chuo hicho Louis Kusaya amesema wanachuo ambao wamehitimu masomo yao wamefundishwa maadili kutokana na kada ambazo wamesomea na kuwataka kuwa mfano mzuri kwenye jamii.
Baadhi ya wahitimu wa chuo hicho mbali na kutoa shukrani kwa elimu waliyoipata, wamesema watasimamia kile ambacho wamefundishwa darasani ili kuhakikisha wanaisadia jamii kuwa na maendeleo mazuri.
Katika mahafali hayo ya 22 zaidi ya wanachuo 193 wamehitimu masomo yao katika kada mbalimbali ikiwemo uuguzi na ukunga, maendeleo ya jamii, ustawi wa jamii na sheria.