Kigoma: Wapigwa faini milioni 4.4 na KUWASA kwa kujiunganishia maji
4 July 2023, 08:59
Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Manispaa ya Kigoma Ujiji, KUWASA imewatoza faini ya shilingi milioni nne na laki nne watu wawili kwa kosa la kujiunganishia maji kinyume na taratibu.
Na, Tryphone Odace.
Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Manispaa ya Kigoma Ujiji, KUWASA imewatoza faini ya shilingi milioni nne na laki nne watu wawili kwa kosa la kujiunganishia maji kinyume na taratibu .
Afisa mahusiano wa mamlaka hiyo Regina Kalima amesema hayo wakati wa oparesheni ya kukagua nyumba ambazo zimeunganishiwa huduma ya maji kinyemela katika eneo la Mkatutu mtaa wa Mlole Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Hatuwezi kuendelea kupata hasara kwa sababu ya watu wanaohujumu miundombinu ya maji
Amesema katika operesheni hiyo wamefanikiwa kukamata nyumba mbili ambazo zimeungnishiwa maji na kuwatoza faini ya shilingi milioni nne na laki nne kama faini kwa kujiunganishia maji bila kibali cha mamlaka hiyo.
Amesema hatua hiyo ya kujiunganishia maji imekuwa ikiwarudisha nyuma kutokana na maji mengi kupotea bila kuingiza pesa wakati wanatumia pes nyingi katika kuboresha miundombinu ya maji.
Baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Mlole wameiomba mamlaka hiyo kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuwabaini watu wanajiunganishia maji kwenye nyumba zao kwani wanaikosesha mapato na kushindwa kujiendesha kwa kufanya ukarabati wa miundombinu ya maji.
Aidha wamesema Serikali kupitia mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira haina budi kuwafuatilia vishoka wanaowaunganishia maji wananchi kwani itasaidia kuokoa pesa zinapotea kutokana na wizi wa maji majumbani.