Joy FM
Joy FM
4 June 2025, 15:32

Wanafunzi wenye ulemavu katika shule ya Kabanga mazoezi wapatiwa msaada wa bima za afya ili kuwasaidia kupata matibabu.
Na Hagai Ruyagila
Katika kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha sekta ya afya nchini, Taasisi ya Usilie Tena yenye makao yake makuu jijini Dar es Salaam, imetoa msaada wa kadi za bima ya afya kwa baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Kabanga Mazoezi, iliyopo katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu, mkoani Kigoma.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi msaada huo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Usilie Tena, Bi. Egra Kamugisha, amesema kutokana na hali duni na kushindwa kumudu gharama ya bima ya afya imepelekea taasisi hiyo kufanya hivyo maana afya bora ni msingi imara wa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Aidha Bi. Kamugisha amesema taasisi yake itaendelea kushirikiana na jamii pamoja na wadau mbalimbali katika kuboresha sekta ya afya, hasa kwa makundi yenye uhitaji mkubwa kama wanafunzi wa shule za msingi mijini na vijijini.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kabanga Mazoezi, Bi. Happiness Boyi, licha ya kuishukuru taasisi hiyo kwa msaada huo ametoa wito kwa wadau mbali mbali wa maendeleo kuendelea kuisaidia jamii isiyokuwa na uwezo.

Naye Timotheo Mapengo, mmoja wa wanafunzi walionufaika na msaada huo, ameilishukuru taasisi ya Usilie Tena kwa moyo wao wa huruma na mchango wa kuboresha maisha ya wanafunzi.
Msaada huo sehemu ya juhudi endelevu za taasisi hiyo katika kuhakikisha watoto wa Kitanzania wanapata haki ya msingi ya huduma za afya bora.
