Wanasiasa marufuku kufanya siasa ndani ya nyumba za ibada
2 October 2024, 16:15
Wakati tukielekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa hapo Novemba mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani, wanasiasa wametakiwa kutotumia nyumba za ibada vibaya ili kuwashawishi waumini kuwachagua katika nafasi mbalimbali.
Na Hagai Ruyagila – Kasulu
Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Western Tanganyika Mhashamu Emmanuel Bwatta amewataka wanasiasa mkoani Kigoma kuacha kutumia nyumba za ibada kama jukwaa la kufanya siasa za kuomba kura badala yake waende kwa ajili ya kuombewa tu.
Askofu Bwatta amesema anaamini suala la siasa liko kwenye maisha yao na tayari ameshaagiza wachungaji wote wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Western Tanganyika kutokubali suala hilo la wanasiasa kutumia nyumba za ibada kufanyia kampeni.
Aidha Askofu Bwatta amewasisita wachungaji hao kuwafanyia maombi tu wanasiasa na siyo vinginevyo.
Kwa upande wao baadhi ya wachungaji wa makanisa ya Anglikana Dayosisi ya Western Tanganyika wamesema watatii maagizo hayo.
Fanueli Kisabo Diwani wa kata ya Murusi kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) amesema wamepokea maelekezo ya Askofu Bwatta lakini viongozi wa dini wanatakiwa kuwa na msimamo ili kuondoa hali hiyo ya kuitumia nyumba ya ibada kama jukwaa la kuombea kura.