Anusurika kufa baada ya kufukiwa na kifusi
12 August 2024, 09:47
Mkuu wa wilaya Kigoma Mh. Salum Kalli amewataka wafanyakazi kwenye miradi mbalimbali ya barabara kuchukua tahadhari wakati wakichimba vifusi ili kuepuka kufukwa kwa maporomoko ya udongo.
Na Tryphone Odace – Kigoma
Mtu mmoja ajulikanaye kwa jina la Michael Christopher fundi ujenzi mkazi wa mtaa wa Kirungu kata ya Machinjioni manispaa ya Kigoma Ujiji Mkoani Kigoma, amenusurika kifo baada ya kufukiwa na kifusi cha barabara wakati akichimba mtaro kwa ajili ya ujenzi wa karavati katika mradi wa barabara ya Kilometa tisa kutoka Katonga kupitia Burega hadi Ujiji.
Kijana huyo ambaye ni Fundi Ujenzi huyo alikumbukwa na tukio hilo eneo la Rutale akiwa katika utekelezaji wa mradi wa barabara hiyo kupitia mradi wa TACTIC unaofadhiliwa na benki ya dunia ambapo baada ya kufikiwa na kifusi wafanyakazi wenzake waliwahi kumuokoa na Kumuwahisha hospitali ya mkoa Kigoma Maweni kwa matibabu.
Mkuu wa wilaya Kigoma, Mh. Salum Kali alitembelea eneo la tukio na kuzungumza na wafanyakazi na wasimamizi wa mradi huo akiwataka kuchukua tahadhari ili madhara yasiweze kutokea kwa watu wanaoshiriki kwenye mradi huo.
Sambamba na hilo Mkuu huyo wa wilaya alitembelea nyumbani kwa majeruhi huyo Mtaa wa Kirugu kata ya Machinjioni manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo alienda kumpa pole na kumjulia hali sambamba na kumpa msaada kwa ajili ya matumizi yake na familia kwa muda wote atakaokuwa nyumbani akipata matibabu.
Akizungumza mbele ya Mkuu wa wilaya aliyemtembelea nyumbani kwa Fundi ujenzi huyo, Michael Christopher alimshukuru Mkuu wa wilaya kwa hatua hiyo ya kumtembelea na kumfariji kwani imemtoa moyo kuona serikali iko Pamoja naye.
Christopher amesema kuwa baada ya kuangukiwa na kifusi na kuokolewa na wenzake alikimbizwa hospitali ya rufaa ya mkoa Kigoma Maweni ambapo alifanyiwa vipimo na kwa sasa anaendelea vizuri.