Wenyeviti wa vijiji na vitongoji watakiwa kutatua kero za wananchi Kasulu
10 January 2025, 13:41
Serikali imesema itaendelea kuhakikisha wananchi wanashirikiana na viongozi wa Serikali za mitaa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kutatua changamoto za wananchi.
Na Hagai Ruyagila – Kasulu
Wenyeviti wa vijiji na Vitongoji halmashauri ya wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wametakiwa kushirikiana kutatua kero za wananchi ili kutekeleza shughuli za miradi ya maendeleo katika vijiji vyao.
Hayo yamebainishwa na Afisa wa serikali za mitaa kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa Kigoma Bw. Hussein Moshi wakati akizungumza na vyombo vya habari baada ya kuhitimishwa kwa semina elekezi kwa wenyeviti wa vijiji na vitongoji yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi.
Bw. Hussein amesema kutokuwa na elimu kwa baadhi ya wenyeviti waliopo madarakani imekuwa chanzo cha ukiukwaji wa sheria wa kanuni za uongozi na kusababisha mwingiliano wa majukumu baina ya wenyeviti wa vijiji na maafisa watendaji wa vijiji hali inayopelekea migogoro na kuzorotesha maendeleo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanal Isaac Mwakisu amewasisitiza kusimamia vyema miradi ya maendeleo iliyopo katika maeneo yao ili iweze kukamilika kwa ubora uliokusudiwa.
Nao baadhi ya wenyeviti wa vijiji na vitongoji wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu wamesema kutokana na kukosa elimu imekuwa chanzo ya migogoro katika vijiji vyao hali ambayo hupelekea baadhi wananchi kususia mikutano ya inayoitishwa na viongozi wao na kwamba mafunzo hayo yataleta tija katika kusimamia shughuli za maendeleo na utatuzi wa kero za wananchi.