Prof. Ndalichako awataka wahitimu wa mafunzo stadi kufanya kazi
18 November 2024, 15:11
Serikali imesema itaendelea kuwasaidia vijana kupitia ujuzi mbalimbali ili kuhakikisha wanapatiwa mikopo itakayowasaidia kujiajiri.
Na Hagai Ruyagila – Kasulu
Wahitimu wa mafunzo ya ufundi stadi Veta wilayani Kasulu mkoani Kigoma wametakiwa kufanya kazi kwa bidii na kuwa na nidhamu ya kazi ili kujiingizia kipato na kujiepusha na vitendo viovu.
Mbunge wa jimbo la Kasulu mjini Profesa Joyce Ndalichako kupitia chama cha mapinduzi CCM amesema hayo wakati wa mahafali ya pili ya chuo hicho kilichopo kata ya Nyumbigwa katika halmashauri ya mji Kasulu.
Profesa Ndalichako amesema vijana wanatakiwa kujituma kwa kufanya kazi na kuwa na nidhamu ya kazi ili kujenga uwaminifu kwa wateja wao.
Kwa upande wake kaimu mkuu wa chuo cha Veta Kasulu Zakaria Mafwele amesema mafunzo mbali mbali waliyoyapata wanachuo hao ikiwemo ufundi umeme, ufundi wa magari pamoja Ushonaji yatawasaidia wahitimu hao kujiajiri au kuajiliwa.
Nao baadhi ya wahitimu wa fani mbalimbali wameeleza namna watakavyo tumia ujuzi walioupata chuoni hapo ili waweze kujiingizia kipato nakuwa mfano wa kuigwa katika jamii inayowazunguka.
Jumla ya wanachuo 89 wanatarajiwa kuhitimu mafunzo hayo ya ufundi wa kozi za muda mrefu ngazi ya cheti sawa na asilimia 81 ya vijana wote waliojiunga na mafunzo ya ufundi stadi mwezi Januari 2023 chuoni hapo.