Joy FM

Madaktari bingwa waweka kambi ya matibabu Kigoma

8 October 2024, 09:54

Katibu tawala wa mkoa wa kigoma Hassan Rugwa akiwa katika hafla ya mapokezi ya madaktari bingwa wa Dkt. Samia mara baada ya kuwasili Kigoma, Picha na Jacob Ruvilo

Baadhi ya wananchi wa  Mnispaa ya Kigoma Ujiji wamepengeza hatua ya ujio wa madaktari bingwa wa Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuwa itasaidia kupata huduma za kibingwa na kuokoa gharama ambazo wangetumia kwenda kutafuta matibabu nje ya mko wa Kigoma.

Na Josephine Kiravu – Kigoma

Madaktari  Bingwa wa Dkt. Samia wameanza Kambi Maalum ya Matibabu ya kibingwa mkoani Kigoma ambapo watatoa huduma za kiafya kwa Siku Saba kuanzia katika Hospitali Nane za Halmashauri za Mkoa wa Kigoma.

Akizungumza kwenye hafla fupi ya mapokezi ya madaktari hao, Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa amesema wananchi wanapaswa kutumia fursa ya uwepo wa kambi hiyo kupata matibabu ya kibingwa jirani na maeneo yao jambo litakalowapunguzia gharama na muda wa kufuata matibabu katika hospitali zilizopo nje ya mkoa wa Kigoma.

Mhe. Rugwa ametoa wito kwa madaktari hao kupitia kazi watakazozifanya mkoani Kigoma kubaini changamoto za utoaji na upatikanaji huduma za kimatibabu zinazoutofautisha mkoa na mikoa mingine kisha kutoa ushauri na mapendekezo ili serikali ya mkoa iweze kuchukua hatua katika kuimarisha utoaji wa huduma za kiafya kwa wananchi.

Sauti ya Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa

Naye Mganga mkuu wa mkoa wa kigoma Dr. Damas Kayera amesema mbali na madaktari bingwa kutoa huduma kwa wananchi watawajengea uwezo madaktari waliopo katika utoaji wa huduma za afya.

Sauti ya Mganga mkuu wa mkoa wa kigoma Dr. Damas Kayera

Kwa upande wake, Mwakilishi  kutoka Wizara ya Afya Jackline Ndanshau amesema kila kituo kitapokea wataalam Saba ikiwa ni pamoja na  Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, watoto na watoto wachanga, usingizi na ganzi, magonjwa ya ndani, upasuaji na mfumo wa mkojo, Daktari bingwa wa Kinywa na Meno pamoja na Muuguzi bingwa.

Sauti ya Mwakilishi  kutoka Wizara ya Afya Jackline Ndanshau

Aidha Ndanshau amesema lengo la serikali ni kuhakikisha huduma bobezi za kibingwa zinawafikia wananchi katika halmashauri zote 184 nchini kuimarisha ujuzi wa wataalam wa Afya kazini pamoja na kuanzisha wodi maalum za watoto wachanga wagonjwa na waliozaliwa na uzito pungufu.