Diwani alia na serikali kushindwa kukarabati barabara Kasulu
2 October 2024, 14:08
Serikali katika halmashauri ya mji wa kasulu Mkoani Kigoma imesema inaendelea kufanya ukarabati wa barabara zilizoharibika na kuzifanyia ukarabati ili ziweze kupitika hasa msimu huu ambao mvua za masika zinapoeleekea kunyesha.
Na Hagai Ruyagila – Kasulu
Diwani wa kata ya Muganza halmashauri ya Kasulu Mji mkoani Kigoma ameilalamikia serikali kushindwa kukarabati miundombinu ya barabara iliyoharibikakatika barabara inayotoka Munganza kuelekea Kabanga ili kuondoa changamoto ya wananchi wanapokuwa katika shughuli zao za uzalishaji mali.
Ameyasema hayo katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya mji Kasulu cha robo ya tatu ya mwaka 2023/2024 ambapo amesema kutokana na barabara hiyo kuharibika imekuwa changamoto kwa wananchi wanapofanya shughuli za uzalishaji mali katika kata hiyo.
Kwa upande wake kaimu meneja wa wakala wa barabara za Mjini na Vijijini TARURA wilaya ya Kasulu Mhandisi Erick Raban amekiri kuharibika kwa miundombinu ya barabara hiyo lakini amesema serikali inaifanyia kazi changamoto hiyo.
Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya Mji Kasulu Noel Hanura ambaye ni diwani wa kata ya Heru Juu amesema mpaka sasa serikali imejitahidi kuboresha miundombinu ya barabara ndani na nje ya halmashauri hiyo licha ya uwepo wa changamoto kwenye baadhi ya miundombinu ya barabara.