Kasulu yafikia lengo uandikishaji daftari la mkazi
22 October 2024, 10:43
Wakati zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la makaazi likifikia tamati oktoba 20, 2024, Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya Kasulu Dkt. Semistatus Mashimba amesema halmashauri hiyo imefikia lengo la zoezi hilo la kijiandikisha.
Na Michael Mpunije – Kasulu
Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma imefanikiwa kuvuka lengo la uandikishaji wa Daftari la makaazi kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa katika halmashauri zote za wilaya hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari msimamizi wa uchaguzi halmashauri ya wilaya ya Kasulu Dkt Semistatus Mashimba amesema licha ya kukabiliwa na Changamoto za umbali wa vituo vya uandikishaji na wanananchi waliongeza vituo vya uandikishaji kwa ajili ya kuwafikia walengwa wote waliokusudiwa na kufanikiwa kufikia malengo waliyojiwekea.
Dkt.Mashimba amewapongeza wananchi, viongozi wa siasa, viongozi wa dini pamoja na vyombo vya habari kwa kutoa elimu kwa wananchi na kufanikisha zoezi hilo.
Kwa upande wake Msimamizi wa uchaguzi Halmashauri ya mji Kasulu Mwl.Vumilia Simbeye amesema zoezi hilo limefanikiwa kwa zaidi ya Asilimia 100 kwenye vituo vyote 117 vya uandikishaji.
Aidha Mwl.Simbeye amesema waliweka malengo ya kuandikisha jumla ya wapiga kura laki Moja,ishirini na mbili elfu na Arobaini na mbili(122042) Baada ya zoezi hilo kutamatika oktoba 20 Jumla ya wapiga kura Laki 1 Ishirini na Tatu elfu,miambili hamsini na nne wameandikishwa(123,254) katika halamshauri hiyo.
Zoezi la uchaguzi wa Serikali za mitaa, unatarajia kufanyika Novemba 27 mwaka huu ambapo wananchi wanatakiwa kushiriki katika uchaguzi huo ili kuwachagua viongozi wenye uwezo wakuleta maendeleo kwa wananchi.