Joy FM
Joy FM
25 September 2025, 08:34

Chama cha ACT – Wazalendo kimeendelea na mikakati ya kuhakikisha kinatatua changamoto zinazowakabili wananchi wake.
Na Tryphone Odace
Mgombea ubunge wa Kigoma Mjini kupitia tiketi ya chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo, mojawapo ya kipaumbele chake cha awali kitakuwa kuboresha miundombinu ya masoko ya jioni yaliyopo katika Kata ya Buhanda, hususan masoko ya Mwansenga na Mgeo.
Akizungumza leo Jumatano, Septamba 24, 2025 kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika eneo la Mwasenga Kata ya Buhanda, Zitto amesema lengo la kuboresha miundombinu ya masoko hayo ili wananchi waweze kufanya biashara zao kwenye mazingira mazuri.

“Kama nilivyoweza kupambania soko la jioni la Marungu lililopo Mwanga kwa uwezo wangu wote na maarifa yangu kutafuta fedha kujenga, ndivyo nitaweza kupambania na haya masoko ya Kata ya Buhanda kwa kuweka taa… ninaweza na nina historia ya kufanya hivi,” amesema Zitto
Zitto ameongeza kuwa akichanguliwa ataweza kushugulikia changamoto ya maji katika kata hiyo ambayo kwa sasa wananchi wake wanapata maji kwa wiki mara moja.
Ameahidi endapo watamchagua atashughulikia swala la Manispaa kugawa viwanja eneo la Masanga mlimani ambapo ni eneo la shughuli ya kuvunja mawe na watu kujipatia kipato.
“ Halmshauri wanapora maeneo hayo na kuyauza ikiwa watu wana leseni ya uchimbaji wa madini ujenzi (kokoto na mawe), nikiwa mbunge nitahakikisha tunafanya uchunguzi kuhusu suala hili ili kuona namna ya kutunza ajira za watu na wakati huo huo kuongeza maendeleo ya makazi,” amesema Zitto.
Mgombea udiwani Mwasenga, Alex Kitumo amesema akichaguliwa watahakikisha wananchi wanapewa mikopo isiyo na riba kwa wananchi wote.
Mjumbe wa Kamati Kuu ACT-Wazalendo Kanda ya Magharibi, Elizabeth Sanga amewatia moyo wananchi hao waliokata tamaa ya kupiga kura kujipanga upya na kujitokeza kwa wingi siku ya Oktoba 29.
Amesema sababu kubwa ya wananchi hao kukata tamaa ni pamoja na kupiga kura kwa kiongozi wanaomtaka lakini matokeo yanatoka tofauti kwa kutangazwa mtu mwingine.
Katibu wa ACT-Wazalendo jimbo la Kigoma Mjini, Idd Adam amesema chama chao kinazungumzia matatizo ya wananchi na jinsi ya kutatua na sio kumzungumia watu au mtu kwenye majukwaa yao.