Joy FM

CHAUMA yaahidi kuboresha huduma za afya na barabara Kigoma

8 September 2025, 12:36

Wananchi wakiwa katika mkutano wa kampeni za chama cha CHAUMA Kata ya Mahembe, Picha na Sadick Kibwana

Kampeni za uchaguzi Mkuu zikiwa zinaendelea vyama mbalimbali nchini vimeendelea kuzunguka kunadi sera na kueleza watakachokifanya iwapo watapewa nafasi ya kuongoza

Na Sadik Kibwana

Chama cha Ukombozi wa Umma CHAUMA kimezindua kampeni zake katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kuomba ridhaa kwa wananchi kuchaguliwa viongozi wa chama hicho ili wakafanye mabadiliko ya kimuundo na kuwaletea wananchi maendeleo katika sekta mbalimbali.

Akieleza  vipaumbele vya Chama hicho, Mgombea wa Ubunge Omar Mussa Mkwarulo akiwa Kata ya Mahembe Jimbo la Kigoma Kaskazini amesema jambo la msingi wananchi watakao piga kura basi ni kupitisha wagombea wa chama hicho wakiwa ni madiwani na Mbunge kwa sababu sera za chama hicho zimejielekeza katika kutatua na kuboresha miundombinu ya barabara, afya na kumaliza tatizo la vitambulisho vya Taifa  Nida ambalo limekuwa kubwa kwa wakazi wa jimbo hilo.

Aidha Mkwarulo amesema ili kufanikisha maendeleo kwa wananchi na kuhakikisha yanapatikana qatahakikisha wanaanza  kuboresha afya za wananchi na atahakikisha maji safi na salama yanapatikana jimboni hapo kwa gharama nafuu.

Baadhi ya wananchi walihudhuria katika uzinduzi wa kampeni za chama cha hicho wamesema wanatamani kuona anatatua changamoto zinazowakabili.

Uchaguzi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuwapata madiwani, wabunge na Rais utafanyika Oktoba 29, 2025 na kauli mbiu ya uchaguzi huo ni  “Kura yako haki yako jitokeze kupiga kura”