Wilaya ya Kibondo yaanza kuwasajili wafanyabiashara wa mazao
28 July 2023, 15:40
Wafanyabiashara wilayani Kibondo mkoani Kigoma wametakiwa kurasimisha taarifa za biashara za mazao wanazofanya ili waweze kutambulika na Wizara ya Kilimo
Na, Tryphone Odace
Halmashauri ya wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma imeanza zoezi la usajili wa wafanyabiashara wa mazao na wenye maghala ikiwa ni utekelezaji wa zoezi la urasimishaji wa biashara za mazao ili kuendana na matakwa ya Wizara ya Kilimo ambayo inamtaka kila mfanyabishara wa mazao kurasimiasha biasahara yake.
Mkuu wa wilaya ya Kibondo Kanali Agrey Magwaza amesema hayo katika kikao na wafanyabiashara wa mazao, wakulima na wamiliki wa maghala ya kuhifadhia nafaka kilichofanyika katika ukumbi wa IOM Kibondo mjini kikiwa na lengo la kuwaeleza zoezi la urasimishaji wa biashara ya mazao kwa kuboresha utaratibu wa uuzaji na ununuzi wa mazao ya kilimo nchini.
Aidha Kanali Magwaza amesema kuwa lengo la serikali ni kuboresha utaratibu huo na kuwalinda wakulima na wafanyabiashara dhidi ya usumbufu na utapeli unaotokea katika biashara ya mazao ya kilimo, kurasimisha sekta ya kilimo ili kuwezesha ufanyaji biashara kwa mujibu wa sheria na taratibu, kuwalinda wafanyabiashara wa ndani dhidi ya wafanyabiashara kutoka nje ya Tanzania wanaonunua mazao moja kwa moja shambani.
Akiwasilisha taarifa ya namna zoezi litakavyoendeshwa, Dkt. Gabriel Chitupila kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kibondo ameeleza kuwa ili kuhakikisha biashara ya mazao ya kilimo inarasimishwa, Wizara ya Kilimo imetengeneza mfumo maalum wa kielektroniki (kidijitali) utakaotumika nchi nzima.
Aidha katika kuutekeleza mfumo huu kwa ufanisi ni lazima mambo matano ya msingi yazingatiwe, ambayo ni usajili wa maghala, usajili wa wafanyabishara ya mazao ya kilimo, usajili wa masoko ya mazao ya kilimo, usajili wa vituo vya ununuzi pamoja na usajili wa vituo vya ukaguzi mazao.