Viwavijeshi vyashambulia mazao ya wakulima Kigoma
18 December 2024, 09:25
Wakulima katika Wilaya za Mkoa wa Kigoma wametakiwa kuzingatia matumizi ya mbegu bora za kilimo zinazohimili magonjwa na kutumia viwatilifu ili kusaidia kukabiliana na wadudu wanaoshambulia mashamba.
Na Kadislaus Ezekiel – Kigoma
Mashamba ya mahindi katika Halmashauri za Wilaya ya Kigoma na Uvinza Mkoani Kigoma yamevamiwa na wadudu maarufu viwavijeshi wasumbufu ambao wanashambulia majani na mimea na kuathiri ukuwaji wa mahindi, ambapo wakulima wameomba hatua za haraka ikiwemo upatikanaji wa dawa za kuua wadudu hao ili kuepusha athari za kukosa mazao ya mahindi.
Wadudu hao maarufu viwavijeshi wasumbufu, hushambulia mmea kwa ndani na majani na kuhafifisha ukuwaji hivyo kuathiri uzalishaji wa mazao.
Wakulima wanalazimika kuomba hatua za haraka, kubaini dawa za kuua wadudu hao ambao wanatajwa kushambulia mashamba ya mahindi.
Katika kikao cha watafiti wa mazao ya kilimo, kutoka taasisi za utafiti wa mbegu za kilimo Tanzania, kituo cha Tumbi Tabora, TARI Kihinga Kigoma pamoja na Makao makuu Dodoma wamewataka wakulima kutumia mbegu bora zinazokinzana na magonjwa na kuepusha mazao kushambuliwa na wadudu, sambamba na kubainisha hatua zinazochukuliwa dhidi ya wadudu wanaoshambulia mazao.