Zaidi ya milioni 400 zajenga daraja, barabara Kigoma
16 September 2024, 10:36
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa Godfrey Mnzava ameutaka uongozi wa halmashauri ya Kigoma kupitia kwa meneja wa wakala wa barabara za mijini na vijijini TARURA kusimamia na kuweka alama kwenye daraja mawe lilipo katika vijiji vya magalaganza na Mweru ili liweze kutudumu kwa muda mrefu.
Wananchi wanaoishi katika maeneo Mgaraganza na Bweru Katika Halmashauri ya Wilaya Kigoma wameipongeza Serikali kwa kuwajengea daraja la mawe ambalo limetajwa kuwa msaada kwa kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa bidhaa.
Wakizungumza na redio Fm, mara baada ya mwenge wa uhuru kuzindua daraja hilo la mawe na barabara wamesema kwa sasa usumbufu wa waliokuwa wakiupata umeisha kwani hapo awali walilazimika kulipia hela ili waweze kubebwa na wakati mwingine mazao yao yakisombwa na maji.
Naye Meneja wa Wakala wa barabara za mijini na vijijini TARURA, wilaya Kigoma Mhandisi Paul Mtapima amesema ujenzi wa daraja hilo la mawe na barabara umegharimu zaidi ya shilingi milioni mia nne hadi kukamilika kwake.
Hata hivyo, Kiongozi wa mbio za mwenge Kitaifa Godfrey Eliakim Mnzava amemtaka Meneja wilaya kigoma kuhakikisha wanasimamia na kulinda matumizi ya daraja hilo ili liweze kudumu kwa muda mrefu.
Mwenge wa uhuru ukiwa katika halmashauri ya wilaya kigoma umetembelea, kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 2, ikiwa na lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.