Migogoro ya kifamilia huathiri malezi na makuzi ya watoto
15 May 2024, 09:40
Serikali ya mkoa wa Kigoma imesema kuwa wazazi kwa kushirikiana na jamii hawana budi kukaa na kutatua migogoro ya familia ili iwe suluhisho la watoto kukua katika maadili na malezi bora.
Na Josephine Kiravu – Kigoma
Katibu tawala mkoani Kigoma Hassan Rugwa amewataka wazazi, walezi na jamii kwa pamoja kushiriki na kujitoa ili kuelimisha na kuhamasisha jamii kufahamu umuhimu wa kutatua migogoro ya kifamilia ambayo mara kadhaa huathiri malezi na makuzi ya watoto.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala mkoa wa Kigoma Hassan Abas Rugwa ambapo pia ameeleza kuwa changamoto za wazazi ndani ya ndoa zisiharibu malezi na makuzi ya watoto kwa ustawi wao wa sasa na wa baadaye.
Pia amesema miongoni mwa changamoto kubwa kwa wazazi au walezi kwa watoto ni kutofustilia mienendo ya watoto wao wanapokuwa mazingira tofauti na nyumbani na kuchukua tahadhari za msingi endapo kutakuwa na tabia isiyoridhisha hasa katika maendeleo ya teknolojia habari na mawasiliano TEHAMA.
Nao baadhi ya viongozi wa dini na wadau mbalimbali wamezungumzia kuhusu kutatua changamoto za malezi kwa watoto ili kutambua majukumu yao kama wazazi au walezi.
Ikumbukwe kuwa tarehe 9 mei ilikuwa ni uzinduzi wa maadhimisho ya siku ya familia ambayo kimataifa maadhimisho hayo hufanyika tarehe 15 mei,na kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya familia duniani ni “Tukubali tofauti zetu kwenye familia ili kuimarisha malezi ya watoto”