Wachungaji walia na ukata makanisani
30 April 2024, 07:22
Ili kuakabiliana na umasikini ambao umekuwa ukisumbua watumishi wa mungu, wameshauriwa kubuni na kuanzisha miradi ya maendeleo ili kuwasaidia kuinua uchumi wao.
Na Hagai Ruyagila – Kasulu
Wachungaji wa kanisa la Anglikana Dayosisi ya Western Tanganyika mkoani Kigoma wameshauriwa kufanya maendeleo ya kanisa na ya kwao binafsi ili kuandaa maisha yao ya kustaafu baada ya utumishi wao.
Hayo yamebainishwa na Mhashamu Baba Askofu wa kanisa la Anglikana Dayosisi ya Western Tanganyika Emmanuel Bwatta wakati wa ibada ya kuwaamuru mashemasi 13 kuwa makasisi katika kanisa kuu la Mtakatifu Andrea Anglikana Kasulu Mjini.
Askofu Bwatta amewasisitiza kuifanya kazi ya Mungu kikamilifu bila kusahau kazi zao binafsi kwa ajili ya maendeleo ya kanisa na yakwao binafsi.
Awali akitoa hotuba ya Neno la Mungu Mchungaji Canon Herman Kapama ambaye ni mwalimu wa chuo cha Lake Tanganyika theological college kutoka Dayosisi ya Western Tanganyika amesema dunia inahitaji viongozi imara ambao wataweza kutatua changamoto zilizopo kwa wananchi ili kuleta maendeleo ndani ya jamii.
Nao baadhi ya Makasisi wapya walioamuriwa katika ibada hiyo akiwemo Mchungaji Fraitony Naftari na Mchungaji Mussa Lutegama wamemshukuru Mungu kwa hatua ya kuwekewa mikono ili kuitenda kazi ya Mungu na kuleta maendeleo ndani ya kanisa na jamii kwa ujumla.