TRA Kigoma yakamata bidhaa feki
2 May 2024, 11:26
Serikali kupitia mamlaka ya mapato imewataka wananchi na wadau mbalimbali ili kusaidia kukabiliana na wimbi la uingizwaji wa bidhaa feki Nchini.
Na Lucas Hoha – Kigoma
Mamlaka ya mapato Tanzania TRA, Mkoa wa kigoma imekamata bidhaa mbalimbali ikiwemo vipodozi na vinywaji ambavyo vimeingizwa nchini kinyume na sheria kupitia mpaka wa Burundi na Tanzania licha ya baadhi ya bidhaa kupigwa marufuku kuingia nchini na shirika la viwango Tanzania TBS.
Hayo yamebanishwa na Meneja wa mamlaka ya mapato Tanzania TRA mkoa wa kigoma Deogratius Shuma wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu bidhaa hizo ambazo zimekamatwa katika wilaya ya buhigwe mkoani kigoma zikitokea nchini Burundi.
Bw. Shuma amesema bidhaa hizo hazikupita kwenye mpaka rasmi kwa lengo la kukwepa kulipa Kodi, huku akiwaomba wananchi kuacha kufanya biashara haramu kwani zinasabisha hasara kwa wananchi na serikali.
Kwa upande wao baadhi ya viongozi wa mamlaka hiyo wamesema kwa mjibu wa sheria zilizopo bidhaa zinapokamatwa wanashirikiana na taasisi nyingine ikiwemo TBS kubaini ni bidhaa zipi zinafaa kwa matumizi na zile ambazo hazifai zinateketezwa kwa moto.
Nao baadhi ya wananchi kutoka mataifa yote mawili yaani Tanzania na Burundi wakizungumza na kituo hiki wakiwa katika kata ya Munanila Wilaya ya buhigwe mkoani kigoma wamekemea tabia ya wananchi kuingiza bidhaa kutoka nchi moja kwenda nyingine kinyume na sheria kwani baadhi ya bidhaa hizo hasa vipodozi hazina sifa kwa matumizi na vimekuwa vikisababisha madhara kwenye ngozi.