Wafanyabiashara Kigoma waikaba shati serikali, wagoma kuhama
29 April 2024, 14:52
Mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali mkoani Kigoma zimesababisha maji kujaa kwenye mwalo na kuharibu miundombinu ya bandari ndogo ya Kibirizi katika Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Na Kadilsaus Ezekiel – Kigoma
Wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi na mbogamboga waliovamiwa na maji kutokana na mvua nyingi kunyesha, katika soko la mwalo wa Kibirizi kata ya Kibirizi Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma, wamelalamikia serikali kushindwa kuwatafutia eneo mbadala la biashara na kulazimika kufanyia biashara pembezoni mwa barabara ya Rasini Kibirizi.
Soko la Mwalo wa Kibirizi linaendelea kujaa maji, yakiwa ni matokeo ya mabadiliko ya tabia nchi na kuathiri shughuli mbalia mbali zikiwemo za kijamii na kiuchumi.
Tayari wafanyabiashara wa mwalo huo, wameondolewa na kutakiwa kuhamia masoko mengine ya kata jirani ya Gungu, agizo ambalo linakumbwa na upinzani kutoka kwa baadhi ya wafanyabaiasha.
Mwenyekiti wa soko la mwalo wa Kibirizi, Khatibu Huseni ameomba serikali kuwapa eneo la Kibirizi Rasini kwa kuwa eneo hilo linafaa kufanyia biashara licha ya kuwa ni eneo la mtu binafsi.
Uongozi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji ulipofuatwa juu ya sauala hilo umesisitiza wafanyabisha wote wa mazao ya uvuvi, wanaoendelea na biashara katika mwalo wa Kibirizi kutii agizo la kuhama kuelekea soko la Masanga.