Mpanda FM

Anusurika Kifo Baada ya Kuchomwa Kisu na Mumewe (Diwani)

03/11/2022, 5:48 AM

KATAVI

Mwanamke anaefahamika kwa majina ya Restuta Januari (Miaka 41) mkazi wa Kata ya Itenka Halmashauri ya Nsimbo mkoani Katavi amenusurika kifo baada ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali maeneo mbalimbali ya mwili wake na anae tajwa kuwa ni mume wake Laulent Mpemba ambaye ni diwani wa kata ya Itenka.

Akizungumza Mpanda redio fm Restuta Ambae amelazwa katika Hospitali teule ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi amesema,kabla ya tukio hilo alikuwa na ugomvi na mume wake kwa muda wa miezi miwili ambapo baadae aliamua kumpisha mumewe huyo na kukimbilia kwa dada yake anayeishi Makanyagio Manispaa ya Mpanda.

Kwa upande wake Dada wa majeruhi Bi. Justina Januari amesema kuwa mdogowake amekuwa na migogoro ya mara kwa mara na mume wake na mara baada ya kumpokea alimtaka arudi kwa mumewe ndipo alipomjibu hawezi kurudi kwa kuwa anatishiwa amani.

Afisa mahusiano hospitali ya rufaa mkoa wa Katavi Emmanuel Tinda amethibitisha kumpokea mgonjwa huyo huku akidai bado anaendelea kupatiwa matibabu hosptalini hapo.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa katavi Ally Hamad Makame amesema uchunguzi bado unaendelea na mara baada ya uchunguzi jeshi litatoa litatoa taarifa juu ya tukio hilo.