Joy FM

Serikali kukamilisha miradi Kigoma

3 April 2025, 16:50

Muonekano wa Meli inayofanyiwa ukarabati ndani ya ziwa Tanganyika, Picha na Mtandao

Serikali ya Tanzania imesema itaendelea kuhakikisha inakamilisha miradi yote ya maendeleo ili kufikisha huduma karibu na wananchi na kuchochea uchumi wa Taifa.

Na Tryphone Odace

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu-Kazi Maalum, George Mkuchika amesema kuwa serikali imedhamiria kutekeleza na kukamilisha miradi yote ya miundo mbinu mkoani Kigoma ili kuiunganisha Tanzania kimataifa.

Waziri Mkuchika amesema hayo Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma akianza ziara ya siku nne mkoani humo kutembelea miradi na kufanya mikutano ya hadhara na wananchi kueleza kazi kubwa inayofanywa na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi.

Muonekano wa bandari ya Kigoma na namna serikali ilivyoboresha huduma, Picha na Mtandao

“haya yote yanayofanyika sasa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi, Rais Samia ametutuma mawaziri wake kutembelea na kukagua miradi na ambayo iko tayari tuizindue iendelee na kazi na hiyo inaonyesha kazi kubwa na iliyotukuka iliyofanywa na Rais wetu”, amesema Waziri Mkuchika.

Katika ziara hiyo Waziri Mkuchika ametembelea mradi wa maboresho na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma, kutembelea bandari ya Kigoma na kukagua utekelezaji wa miradi ya ukarabati wa meli za Mv.Liemba na MT Sangara na kusema kuwa miradi yote ambayo serikali inatekeleza itakamilishwa.

Muonekano wa bandari ya Kigoma na namna serikali ilivyoboresha huduma, Picha na Mtandao