

1 April 2025, 15:16
Baada ya Serikali kuanza ujenzi wa reli ya kisasa SGR kutoka Tabora – Kigoma wananchi wameanza kunufaika na ujenzi kupitia miradi mbalimbali inayojengwa karibu na vijiji reli hiyo inapopita.
Na Tryphone Odace – Buhigwe
Wananchi wa jimbo la Buhigwe wilaya ya Buhigwe Mkoani Kigoma wanatarajia kunufaika na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Uvinza mkoani Kigoma hadi Msongati nchini Burundi ambapo miradi mbalimbali ya kijamii ikiwemo soko la Kimataifa la ujirani mwema litajengwa.
Mbunge wa jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma, Felix Kavejuru alisema hayo akihutubia mkutano wa hadhara wa wananchi katika kijiji cha Kilelema wilaya ya Buhigwe mpakani na nchi ya Burundi na kuwataka wananchi hao kujiandaa kwa biashara kubwa ambayo itabadilisha maisha yao kwa kiasi kikubwa.
Kavejuru amesema kuwa pamoja na soko hilo la ujirani mwema pia litajengwa daraja katika mto Malagarasi kuunganisha kijiji hicho na mikoa ya Burundi kwa barabara ili kurahisha shughuli za biashara baina ya wananchi hao wa wilaya ya Buhigwe na mikoa mingine ya Burundi.
Kutokana na hilo Mbunge huyo amewataka wananchi wa vijiji hivyo vya mpakani na wilaya nzima ya Buhigwe kujiandaa kwa kulima mazao mbalimbali ambayo yatakuwa biashara kubwa nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ambapo reli hiyo itafika kutokana na mahitaji makubwa ya bidhaa za kilimo katika nchi hizo.
Baadhi ya wananchi wa jimbo hilo akiwemo Mathias Ilankunda akiongea na waandishi wa habari baada ya mkutano huo ameishukuru serikali kwa kupitisha reli hiyo kwenye kijiji chao lakini wameitaka serikali kuwasirikisha kwa karibu ili kunufaika kwa vitendo badala ya maneno ya sasa na mradi ukianza fursa hizo wanapewa watu kutoka mbali na kijiji chao.