DC Kasulu akabidhiwa mradi wenye thamani ya milioni 35 na NRC
17 December 2024, 09:31
Shirika la NRC limemkabidhi mradi wa matundu sita ya vyoo vya kisasa kwa mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanal Isaac Mwakisu yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 35 yatakayotumiwa na Wanafunzi wakike wa shule ya msingi Tulashashe iliyopo Halmashauri ya Mji Kasulu.
Mratibu wa miradi ya maji na usafi wa mazingira (WASH) kutoka shirika la NRC Mhandisi Denis Arbogast akimkabidhi mkuu wa wilaya ya Kasulu mradi wa vyoo vya kisasa na kuwa moja ya juhudi za maendeleo wanazozifanya ni kuhakikisha wanapata fedha kwa ajili kutatua baadhi ya changamoto kwa jamii ambapo wamejenga matundu hayo ya vyoo kwa ajili ya watoto wakike ili kuwasaidia katika maendeleo yao ya elimu.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanal Isaac Mwakisu licha ya kulishukuru shirika hilo ameliomba kuwajengea pia watoto wa kiume vyoo vya kisasa sambamba na kumtaka mwalimu mkuu wa shule hiyo kuhakikisha wanaitunza miundombinu ya vyoo hivyo.
Naye mwalimu mkuu wa shule ya msingi Tulashashe Mwl, Yasini Sunzu amesema atahakikisha wanaitunza miundombinu ya vyoo hivyo maana uwepo wake katika shule hiyo itaongeza morali ya mahudhurio ya wanafunzi na ufaulu katika masomo yao.
Shule ya msingi Tulashashe ina jumla ya wanafunzi 586 huku wakike wakiwa 335 na wakiume wakiwa 251.